Sunday, February 24, 2013

HISTORIA YA MTWARA


Na Cosmas J. Pahalah

Mkoa wa Mtwara ni wapili kwa udogo baada ya Mkoa wa Kilimanjaro.Jina la Mtwara limetokana na neno la lugha ya kimakonde “kutwala” ikiwa na maana ya kuchukua(kunyakua) kitu chochote na linatumika kwa maeneo matatu tofauti ambayo ni:
Mtwara Jina la Mkoa, Mtwara-Jina la mji mkuu na makao makuu ya Mkoa, Mtwara-Wilaya na makao makuu ya Wilaya ambayo kiutawala kuna Mtwara vijijini na Mtwara Mikindani
Wakati wa utawala wa Waingereza Tanganyika ilikuwa na majimbo 8. Mkoa wa Mtwara umechotwa kutoka eneo kubwa la Tanzania ambalo wakati wa utawala wa Waingereza liliitwa jimbo la kusini. Jimbo la kusini lilijumuisha Mikoa mitatu ya sasa Lindi,Ruvuma na Mtwara.
Jimbo la Kusini lilijumuisha Wilaya 8 ambazo ni Mtwara, Newala, Masasi, Lindi, Kilwa, Nachingwea, Tunduru na Songea.
 Mkoa wa Ruvuma ndio ulikuwa wa kwanza kugawanywa toka Jimbo la Kusini mnamo miaka ya 1960. Mwaka 1971 Jimbo la Kusini liligawanywa tena na kuundwa rasmi kwa Mikoa ya Mtwara na Lindi.
Mtwara ikiwa na Wilaya 3 kwa wakati huo ambazo ni Mtwara, Newala na Masasi. Kwa sasa Mtwara inaundwa na Wiliya 5 ambazo ni Mtwara, Newala, Masasi, Tandahimba na Nanyumbu. Makabila yaliyokuwemo katika jimbo hilo ni wangoni ,wamatengo, wandendeule ,wamatumbwi, wamwera,wamagingo,wamakonde,wayao na wamakua ambayo yamekuwa na uhusiano mrefu wa jadi na nyingi za mila na desturi zao kwa ujumla zinalingana mno.
Baada ya kuundwa kwa Mkoa wa Mtwara makabila makubwa matatu yanayopatikana ni Wamakonde, Wamakua na Wayao wanaopatikana katika Wilaya tofauti za Mkoa huu. Hata hivyo Wamakonde wanapatikana zaidi katika Wilaya za Newala na Mtwara, Wamakua na Wayao wanapatikana zaidi Wilaya ya Masasi.
 


Kusini chini ya Waingereza
Baada ya Wajerumani kuangushwa duniani pote katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia (1914 – 1918), Tanganyika, iliyokuwa sehemu ya Dutch East Africa (nchi nyingine katika eneo hili zikiwa Rwanda na Burundi) iliwekwa chini ya utawala wa Waingereza kama wadhamini.

Nchi haikuwa koloni kama ilivyokuwa Kenya, Nyasaland( Malawi) na Northern Rhodesia (Zambia). Kwa maeneo ya kusini hali ilikuwa kama Wadachi waliwaambia cha kuwafanyia wenyeji wa kusini.
 Hakuna kumbukumbu zinazoonyesha kwamba watawala wapya walikuwa na mipango au azma ya kuendeleza eneo hilo katika fani mbali mbali. Yaliyotokea yalilenga kunufaisha watawala.
Baada ya vita Waingereza walikuwa wachovu kiuchumi hali ya huduma za kijamii ziliathirika na vita. Kampuni iliyoitwa Overseas Food Corporation ilianzisha mradi mkubwa wa kulima karanga Urambo (Tabora) Kongwa (Dodoma) na Nachingwea (Lindi).
 Ili kuhudumia mashamba kwa ufanisi bandari ya Mtwara iliboreshwa. Wakati huo huo wakajenga reli na bomba la mafuta toka bandarini Mtwara hadi Nachingwea. Reli ilikuwa ienddelee hadi Mbamba bay pwani ya ziwa Nyasa.
Mnamo mwezi Oktoba 1961 lilifunguliwa tawi la reli la kilomita takribani 40, toka Chilungula hadi Masasi.
 Miundombinu na shughuli za kilimo zilitoa ajira na maeneo yaliyopitiwa na miundo msingi hiyo yalifunguka kwa maendeleo

Kwa sababu mbali mbali mradi wa karanga Nachingwea ulifungwa. Mwaka mmoja baada ya Tanganyika kupata Uhuru, sarikali ya Tanganyika huru ikaamini kuwa reli na bomba la mafuta vilikuwa ni miradi isiyo na tija. (white elephant).

 Reli na bomba vikang’olewa. Athari za hatua hiyo ni bayana .Kusini kulizidi kuzama kimaendeleo, taswira iliyodumu kwa kipindi kirefu. Lakini kwa muda mfupi watawala (Waingereza) walimaizi kwamba eneo la kusini lilikuwa na utajiri mwingi hivyo wakaita “Cinderella Province” Cinderella ikiwa na maana ya ‘mtu au kitu ambacho uzuri au uwezo wake haujatambulikana”.
Jingine walilolifanya Waingereza ni kuangusha magogo na kupasua mbao huko Rondo Mnara (Lindi vijijini). Kampuni iliyoitwa Steel Brothers ilifanya kazi hiyo miaka ya 1950. Wakavuna , wakachuma na kuondoka . Wananchi wakaachiwa visiki vya mipingo , mbambakofi,mivule nk. wakati huo huo walikumbatia umasikini.

Kusini baada ya uhuru.

Miaka michache ya kuelekea uhuru kulianzishwa mradi mkubwa wa maji toka mto Ruvuma ,uliendeshwa na kampuni ya Makonde Water Corporation. Ilipangwa maji yaenezwe sehemu mbalimbali huko kusini. Miaka michache baada ya kuasisiwa kwa vishindo mradi ulikufa. Wananchi hawakuelezwa sababu za mabadiliko hayo.

Madhila,taabu na kero za kukosa maji hazikumilithika .
Katikati ya miaka 1960 kulizuka mgogoro wa kiwanja katika mji mdogo wa Mahuta (wakati huo Newala , sasa uko katika wilaya ya Tandahimba ).
Mfanyabiashara wa Kiasia alipora eneo hilo ili ajenge kituo cha mafuta ya nishati. Wananchi wakachachamaa. Uongozi wa mkoa na wilaya ukaingilia kati. Kwenye mkutano wa hadhara hapo Mahuta , kiongozi wa wananchi alipigwa viboko kwa sababu za “kupinga hatua za maendeleo “ kama walivyoita watawala.
Kupinga uonevu kunyanyaswa na kudharauliwa, wananchi waliandika barua ngazi za juu za taifa na kudai , moja , mkuu wa mkoa na yule wa wilaya wahamishwe ,mbili, wapendekeze majina ambayo yatatoa mkuu wa mkoa na yule wa wilaya ; na tatu kama maombi hayo hayatakubalika watajitenga na kujiunga na Msumbiji ili wawe pamoja na FRELIMO kutafuta ukombozi. Yaliyofuata ni historia.
Miaka mitatu baada ya uhuru wa Tanganyika , wana Msumbiji kupitia FRELIMO walianzisha vita vya ukombozi. Kutokana na mazingira ya kijiografia ( kati ya nchi mbili ) eneo lote la kusini likawa “no go area” – hapakuwa na shughuli zozote za maana za kimaendeleo zilizokuwa zikifanyika .
 FRELIMO wakafanikiwa kukunja jamvi ukoloni mwaka 1975. Ni dhahiri kwa miaka kumi wengine walikuwa wamesonga mbele hapa nchini . Mategemeo na matumaini ya wengi huko kusini ni kuwa serikali ingekuwa na programu maalum “kufidia muda uliopotea”. Wakati wa Vita kuu ya Pili vya dunia Yugoslavia ilipambana na majeshi ya Adolf Hitler .
Marshal Josef Tito akawaambia wapiganaji wale “ The wounded should not be left behind “ ( majeruhi wasiachwe nyuma). Kimaendeleo kusini ilijeruhiwa na kuachwa nyuma.
Barabara ya Dar es salaam – Lindi ni “mkunga” wa matatizo ya kusini.
Ahadi za serikali kuijenga zimechukua kipindi kirefu kutekelezwa. Miaka ya 1970 – 80 kampuni moja ya Kitanzania na taasisi moja ya serikali waliteuliwa kujenga barabara hiyo.
 Wakajenga makambi Nangurukuru (Kilwa).Hakuna ushahidi wa kazi iliyofanywa – tatizo la barabara likawa “ kichwa cha mwenda wazimu”. Mwaka 1977 wananchi wa kusini, wakiungwa mkono na wa maeneo mengine, waliasisi mchango maalum kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo. Mwitikio wa wito huo ulikuwa chanya.
Ofisini ya Waziri Mkuu ikasitisha zoezi hilo kwa ahadi kuwa serikali igejenga mradi huo. Imechukua miongo kadhaa kukamilika kazi hiyo.
Miaka ya 1960 – 70 wananchi wa kusini walihamasishwa kulima korosho kwa ajili ya biashara. Matokeo yalikuwa ya kutia moyo. Mapori yalipisha mashamba ya mikorosho. Zao likachangia umasikini. – Pembejeo bei juu na soko likawa halina uhakika .
Kuna viwanda vya kubangua korosho Masasi , Newala Lindi na Mtwara lakini hakuna msimamo maalum wa Bodi ya Korosho na wanasiasa wa kuuza nje zao lililoongezewa thamani. Bado wanakumbatia fikra hafidhina zilizopitwa na wakati wa kuuza nje ya nchi korosho ambazo hazijabanguliwa.

No comments:

Post a Comment