Sunday, February 24, 2013

MAGONJWA HAYA CHANZO CHA MIKOROSHO KUDUMAA

KOROSHO ni zao muhimu la biashara katika nchi yetu kwani linampatia mkulima kipato na kuliingiza taifa fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya zao hilo ndani na nje ya nchi. Kwa kawaida miti ya mikorosho inastawi vizuri katika ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi. Zao hilo hapa Tanzania linalimwa na wakulima wadogo ambao wana miti mikorosho kati ya 60 mpaka 80.
Mikoa inayolima korosho ni Mtwara, Lindi, Pwani, Tanga na Ruvuma katika wilaya ya Tunduru. Mikoa mingine ambayo imeanza kulima korosho kwa kiwango kidogo katika maeneo yenye hali ya hewa inayofaa kwa kilimo cha zao hilo ni mkoa wa Mbeya, Njombe, Iringa, Morogoro, Dodoma, na Singida.
Uzalishaji wa juu wa korosho katika msimu wa mavuno wa mwaka 1973/74 ulifikia tani 145,000 za korosho ambazo kwa sehemu kubwa zilisafirishwa kwenda India.
Magonjwa ni kikwazo
Mbali na hayo zipo changamoto mbalimbali ambazo zinasababisha baadhi ya wakulima kukata tamaa kwa mfano kuwapo kwa ugonjwa unaoshambulia zao hilo.Mkoani Mtwara, kuna kituo cha utafiti wa magonjwa yanayoshambulia zao hilo cha Naliendele ambacho kinafanya utafiti ili kubaini magonjwa na wadudu waharibifu, na kutafuta ufumbuzi.
Dk Louis Kasuga ni mtafiti wa kituo hicho anasema ugonjwa wa Ubwiri, ulionekana ni tatizo kubwa katika kilimo cha korosho. Katika Miaka ya karibuni pia ugonjwa wa blaiti nao umeonekana kushambulia zaidi zao hilo na kwamba hivi sasa magonjwa hayo yamepatiwa dawa za kudhibiti magonjwa hayo.
Dk Kasuga anasema tatizo lingine ni gugu tegemezi (dodder) ambalo limekuwa likiota kwenye maeneo ya Mtwara, Lindi, Kilwa, Rufiji, Mkuranga, Bagamoyo, Pangani, Tanga na Mkinga. Gugu hilo ni chanzo chake ni mbegu iliyoota na kutegemea mmea mwingine kama miti ya mikorosho kustawi.
Utafiti uliofanywa na Kituo cha Naliendele kwa kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umethibitisha kuwa gugu hilo linastawi vizuri katika ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi. Dk Kasuga anasema mbali ya gugu hilo kushambulia mikorosho pia linashambulia mazao mengine kama michungwa, miti ya membe, mimea mingine.
Wakulima wanatambua kuwapo kwa tatizo hilo, lakini uelewa kuhusu chanzo cha tatizo hilo numekuwa ni utata na namna ya kudhibiti bado limekuwa ni kitendawili.
“Gugu hilo halina majani hivyo halina uwezo wa kujitengenezea chakula chake chenyewe, kwa msingi huo huishi kwa kutegemea mimea mingine ili liweze kupata chakula ikiwa ni pamoja na miti ya mikorosho,” anasema mtaalamu huyo.


Gugu lapunguza uzalishaji
Anasema gugu hilo linadumaza na kunyonya chakula cha mimea mingine na kwamba gugu hilo linaweza kusababisha mmea kufa au kukauka. Dk Kasuga anasema gugu hilo linasambaa kwa urahisi zaidi kwa njia ya upepo, maji, ndege, na wanyama. 
Anasema gugu hilo linapunguza uzalishaji wa korosho kwa asilimia 100 kwa sababu linategemea miti ya mikorosho kupata chakula. 
“Hii ni kwa sababu ya ushindani wa chakula, maji na jua naa gugu hilo linakuwa na lina nguvu kubwa ya kunyonya maji na chakula kutoka katika mti wa mkorosho, hali hiyo inapunguza kipato cha mkulima kutokana na kushuka kwa mavuno ya korosho,” anasema. Anasema gugu hilo linasababisha umaskini wa kipato na chakula katika kaya na kupunguza kipato cha fedha za kigeni kwa taifa. 
Anabainisha kwamba mbegu za gugu tegemezi zinauwezo wa kukaa chini ya ardhi kwa miaka kumi bila kupoteza uwezo wa kuota na hivyo linaonekana kuwa sugu. Kwa mujibu wa tovuti mbali mbali, mbegu za gugu tegemezi ni ngumu kufa kwani hata wanyama wakila na kutoa kinyesi zinauwezo wa kuota.

Dk Kasuga anasema njia za kudhibni gugu hilo ni kutoa kambakamba zake kwa kuzivuta, ingawa gugu hilo limekuwa likirejea kwenye mti uliopo karibu na gugu. Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Pwani, Robinso Wanjara anasema uongozi wa Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na kituo cha utafiti cha magonjwa ya korosho kimewapa maelekezo maofisa kilimo ngazi za kata ili wakachungeze ukubwa tatizo hilo.
“Tunaamini kuwa wataalamu wetu tuliowatuma kwenda kwa wakulima watatuletea takwimu sahihi na kuzipeleka kwenye kituo cha Naliendele kwa ajili ya utafiti zaidi,” anasema Wanjara.
Anasema kutokana na kuwapo kwa gugu hilo katika Mkoa wa Pwani, anasema kuwa kiwango cha uzalishaji kimekuwa kikisuasua na kusabaisha wakulima kupata mavuno kidogo.
“Katika mkoa wetu huu wa Pwani zao tunalolitegemea kwa ajili ya biashara ni korosho likifuatiwa na muhogo, matunda, na mbogamboga sasa linavyoathiriwa na gugu hilo linasababisha Mkoa wa Pwani uathirike kimapato,”amesema.


Wakulima wazungumzia gugu tegemezi
Niliweza kupata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wakulima wa zao la korosho kutoka katika Kijiji cha Malendego kilichoko Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi juu ya namna wanavyolitambua hili gugutegemezi na njia wanazozitumia katika kukabiliana nalo Mkulima wa Kijiji cha Malendego wilayani Kilwa, mkoani Lindi, Omary Mtunyungu anasema gugutegemezi limemuathiri kiuchumi na kwamba umasikini unabisha hodi katika familia yake.
Mtunyungu anasema kutokana na hali hiyo ametoa taarifa kwa wataalamu wa kilimo ili kupata msaada wa ufumbuzi, lakini mpaka sasa tatizo halijatatuliwa.
“Inaonekana idadi ya wataalamu wa kilimo ni ndogo kwa sababu sisi wa huku kijijini hatufikiwi na huduma hiyo naomba serikali ijitahidi kuongeza idadi ya wataalamu ili watusaidie jinsi ya kukabiliana na vikwazo vya kilimo hasa magonjwa .
Mkulima na mkazi wa Kijiji hicho cha Malendego, Mohamedi Mtauka anasema amekata tamaa kuongeza kilimo cha zao hilo kwa kuwa gugutegezi limeathiri sana mimea yake ya korosho na kusababisha kipato chake kushuka.
Asili ya kilimo cha zao la korosho ni kutoka nchi ya Brazil iliyopo Amerika ya Kusini na liliingizwa Tanzania katika karne ya 16 kutokea Msumbiji ambako lilikuwa likilimwa na Wareno.

No comments:

Post a Comment